Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa WFP apaazia sauti ukata wa usaidizi kwa wakimbizi wa Syria

Mkuu wa WFP apaazia sauti ukata wa usaidizi kwa wakimbizi wa Syria

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, Ertharin Cousin, ameeleza kutiwa hofu na hali inayozorota ya wakimbizi wa Syria walioko Jordan, baada ya ziara yake katika ufalme huo.

Akiwa Jordan, Bi Cousin amekutana na familia za Wasyria na kuwasikiliza wakielezea matumaini na hofu yao, hususan vijana ambao wanahaha kupata chakula na wengine wakihofia kuangamizwa kwa ndoto zao iwapo hawatarudi shule.

Ziara ya Bi Cousin pia imefuatia kupunguzwa kwa kiwango cha usaidizi unaotolewa na WFP kwa Wasyria wapatao nusu milioni, ambao wanaishi nje ya kambi za wakimbizi nchini Jordan, kwa sababu ya uhaba wa ufadhili.

Bi Cousin ametoa wito kwa jamii ya wahisani watambue taabu ya watu wa Syria na kuendelea kutoa kwa ukarimu ili wadau wa kibinadamu waweze kuwasaidia hadi pale watakaporejea makwao.