Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asikitishwa na hali ya ufadhili kwa UNRWA

Ban asikitishwa na hali ya ufadhili kwa UNRWA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ameelezea kusikitishwa mno na hali ya kifedha inayolikabili Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwasaidia Wapalestina, UNRWA, pamoja na madhara ya kibinadamu, kisiasa na kiusalama yatakayotokana na hali hiyo, iwapo ufadhili wa kutosha na endelevu hautatolewa mara moja kwa mwaka 2015 na baadaye.

Ban amesema hayo katika barua yake ya kuwasilisha ripoti ya Kamishna Mkuu wa UNRWA kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa wakati huu ambapo mizozo na taabu kwa wanadamu ikiongezeka kote Mashariki ya Kati, ni lazima UNRWA - ambayo ndiyo nguzo ya ustawi kwa idadi ya Wapalestina milioni tano waliosajiliwa – iendelee kupewa rasilmali zinatakazoiwezesha kuendelea kutoa huduma, zikiwemo za elimu kwa watoto wakimbizi wa Kipalestina nusu milioni.

Ameunga mkono pendekezo la Kamishna Mkuu wa UNRWA la kuhakikisha hali tete iliyosababishwa na uhaba wa ufadhili kwa UNRWA mwaka 2015 inakabiliwa mara moja, na kushughulikia masuala ya ufadhili ya mara kwa mara yanayolikabili shirika hilo kwa mwaka 2016 na baada ya hapo.

Ban ametoa wito kwa wahisani wafanye hima kuhakikisha kuwa dola milioni 100 zinazohitajika zinatolewa kwa UNRWA haraka iwezekanavyo, ili watoto wa Palestina waanze shule kwa mwaka 2015-2016 bila kukawia.