Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande kinzani Yemen zisilenge maeneo ya kiraia- UM

Pande kinzani Yemen zisilenge maeneo ya kiraia- UM

Ofisi ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, imeeleza kusikitishwa na mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia nchini Yemen, yakiwemo maeneo ya ibada, hospitali na shule.

Taarifa ya Ofisi ya Haki za Binadamu imesema kuwa idadi ya raia waliouawa nchini Yemen imefikia 1,916, huku raia wengine 4,186 wakiwa wemejeruhiwa tangu kuongezeka kwa mapigano ya silaha mnamo tarehe 26 Machi.

Akiongea na waandishi habari mjini Geneva, msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, Cecile Poully ametoa maelezo zaidi

Katika majuma machache yaliyopita, kumekuwa na machambulizi mawili yaliyosababisha maafa hasa katika maeneo ya makazi ya raia. Mnamo Julai 19, raia 95 waliuawa, wakiwemo watoto 29, na 198 kujeruhiwa katika eneo la makazi la Al Ghaleel, mjini Aden. Mnamo Julai 24, raia wapatao 73 waliuawa, wakiwemo watoto 11, na raia 93 kujeruhiwa, wakati nyumba mbili za makazi ziliposhambuliwa eneo la Taiz. Tunajaribu kuthibitisha vyanzo vya mashambulizi hayo.”

Ofisi hiyo imetoa tena wito kwa pande zote kinzani zihakikishe kuwa zinatofautisha kati ya malengo ya kiraia na kijeshi, na kufuata kanuni za kusawazisha nguvu wakati wa operesheni za kijeshi, na kuchukua tahadhari zote ziwezekanazo ili kuepusha au kupunguza athari za ghasia dhidi ya raia.