Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuanza kesi ya Hissène Habré ni hatua kubwa kwa haki Afrika- Kamishna Zeid

Kuanza kesi ya Hissène Habré ni hatua kubwa kwa haki Afrika- Kamishna Zeid

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein, amekaribisha kufunguliwa mashtaka  dhidi ya rais wa zamani wa Chad, Hissène Habré, mbele ya mahakama maalum nchini Senegal, akitaja tukio hilo kama hatua kubwa kwa haki barani Afrika.

Amesema kufunguliwa kwa mashtaka dhidi ya Bwana Habré miaka 25 baada ya kuondoka mamlakani na kukimbilia Senegal, ni muhimu kwani inaonyesha kuwa viongozi wanaotuhumiwa kwa uhalifu mbaya sana wasidhani kuwa watakwepa mkono wa sheria milele.

Mnamo Agosti 22, makubaliano yalisainiwa kati ya Senegal na Muungano wa Afrika, AU kuanzisha mahakama maalum katika mfumo wa sheria wa Senegal ili kuwashtaki washukiwa wa uhalifu wa kimataifa uliotendwa nchini Chad kati ya mwaka 1982 na 1990, ukiwemo mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita na utesaji.

Cécilé Pouilly ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, Geneva

“Ili amani ya kijamii idumu, ni lazima kumulika kilichotokea wakati wa uongozi mbali mbali ambapo ukiukaji mkubwa wa binadamu ulitendeka, kwa mfano chini ya uongozi wa Habré. Ni lazima waliowajibika wapelekwe mbele ya sheria. Hiyo itawezesha nchi kusonga mbele.”