Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kubana matumizi ya serikali Ugiriki kusibinye haki za binadamu – Mtaalam wa UM

Kubana matumizi ya serikali Ugiriki kusibinye haki za binadamu – Mtaalam wa UM

Mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa ameonya leo kuwa hatua zinazotarajiwa za ubanaji wa matumizi ya serikali ya Ugiriki, ziangaliwe vyema zisije zikasababisha ukiukwaji wa haki za binadamu. Taarifa kamili na Joshua Mmali

(Taarifa ya Joshua)

Juan Pablo Bohoslavsky, ambaye ni mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu deni la kigeni na haki za binadamu, ametoa wito kwa taasisi za Ulaya, Shirika la Fedha Duniani, IMF na serikali ya Ugiriki zitathmini athari za hatua za ubanaji matumizi ya serikali, ambazo zinatarajiwa kuchukuliwa kama sehemu ya makubaliano mapya ya kuikwamua Ugiriki, ambayo uchumi wake umedorora.

Akiwa mjini Addis Ababa, ambako anahudhuria kongamano la kimataifa kuhusu ufadhili kwa maendeleo, Bwana Bohoslavsky amesema anatumai kuwa makubaliano hayo yaliyofikiwa mjini Brussels Ubeljiji, yataepusha maafa zaidi nchini Ugiriki.

Amesema sera za kubana matumizi zaidi zinapaswa kuheshimu haki za binadamu, na kwamba la kipaumbele liwe ni kuhakikisha kuwa kila mtu nchini Ugiriki anafurahia haki zake za kiuchumi, kijamii, na kitamaduni, pamoja na haki ya kupata huduma za afya, chakula na usalama wa kijamii.