Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zaafikia kufadhili ajenda mpya ya maendeleo endelevu

Nchi zaafikia kufadhili ajenda mpya ya maendeleo endelevu

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, leo zimeafikia makubaliano ya kihistoria kuhusu msururu wa hatua mathubuti za kubadili mifumo ya fedha duniani na kubuni uwekezaji wa kukabiliana na changamoto kadhaa za kiuchumi, kijamii na mazingira.

Makubaliano hayo yamefikiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia na nchi 193, kufuatia mashauriano yaliyoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Tedros Adhanom Ghebreyesu, wakati wa kongamano la tatu kuhusu ufadhili kwa maendeleo, ambalo limekuwa likifanyika tangu mwanzoni mwa wiki hii.

Makubaliano hayo yaitwayo, Ajenda ya Addis Ababa ya Kuchukua Hatua, yanatoa msingi wa kutekeleza ajenda ya kimataifa ya maendeleo endelevu, ambayo viongozi wa dunia wanatarajiwa kupitisha mnamo mwezi Septemba mwaka huu.

Makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha ubia wa kimataifa, ambayo imefikiwa baada ya miezi ya mashauriano yenye lengo la kuwa na maendeleo jumuishi ya kiuchumi na kuboresha maisha ya watu, na wakati huo huo kulinda mazingira.

Katibu Mkuu Ban Ki-moon ameyataja makubaliano hayo kama hatua muhimu katika kujenga mustakhabali endelevu kwa wote, kwani yanaweka mkakati wa ufadhili kwa maendeleo endelevu.