Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo hupaswa kuangaziwa kwa mtazamo wa mbali: Eliasson

Mzozo hupaswa kuangaziwa kwa mtazamo wa mbali: Eliasson

Viongozi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa na wadau wamekutana leo kwenye kikao cha mwaka kuhusu mfuko wa ujenzi wa amani, ambapo wametathmini mafanikio ya mfuko huo ambao unafadhili zaidi ya  miradi 200 katika nchi 22 zinazojikwamua baada ya vita.

Akifungua rasmi kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amesema amefuraishwa na mafanikio ya mfuko huo katika kuimarisha mamlaka za serikali baada ya vita, akizingatia masomo yaliyofundishwa  na utekelezaji wa miradi hii, yakiwa ni umuhimu wa uongozi mzuri kwenye nchi husika, umiliki wa utaratibu huo na jamii yenyewe, ushirikishaji wa wanawake na umuhimu wa kuwa na makubaliano jumuishi ya amani kabla ya kuanza ukarabati.

Akisikitishwa na upungufu wa ufadhili kwa mfuko huo, amekariri wito wake:

“Tunapaswa kukumbuka kwamba maisha ya mzozo ni pamoja na muda kabla ya kuanza mzozo na baada ya mzozo. Huwezi kumuacha  mgonjwa aliyepasuliwa moyo arejee kazini kesho yake, si ndiyo? Kuna haja ya kumpatia muda wa kupata ahueni, yaani muda wa maridhiano na ukarabati wa mamlaka za serikali. Tunapaswa kuona maisha ya mzozo kwa mtazamo wa muda mrefu, si muda ule mfupi ambapo tunaona picha za vita kwenye runinga.