Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kasi ya ukimbizi yaongezeka uwezo wa kuhudumia ukidumaa:UNHCR

Kasi ya ukimbizi yaongezeka uwezo wa kuhudumia ukidumaa:UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema matukio ya vita, mizozo na mateso yanayoendelea sehemu mbali mbali ulimwenguni yamesabibisha idadi kubwa ya wakimbizi ambayo haijawahi kutokea duniani. Assumpta Massoi na maelezo kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya UNHCR kuhusu mwelekeo wa wakimbizi duniani iliyotolewa leo kuelekea siku ya wakimbizi duniani tarehe 20 mwezi huu.

Mathalani inasema mwishoni mwa mwaka 2014 takribani watu Milioni 60 walikimbia makwao ikilinganishwa na Milioni 37 na Nusu muongo mmoja uliopita, ikieleza kuwa kasi ya ukimbizi ilizidi tangu mwanzoni mwa mwaka 2011, kufuatia mzozo wa Syria.

Kamishna Mkuu wa UNHCR Antonio Guterres akizungumza mjini Istanbul, Uturuki amesema hali hiyo haikubaliki akitaka hatua zichukuliwe kuondokana na matukio  yanayosababisha ukimbizi.

Amesema duniani hivi sasa , mtu mmoja kati ya 122 ni mkimbizi au anasaka hifadhi ugenini wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa na wadau wake wa misaada hawana uwezo wa kukidhi mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka kila uchao.