Ban aunga mkono waraka wa Papa Francis kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Ban aunga mkono waraka wa Papa Francis kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha waraka wa mkuu wa kanisa katoliki duniani Papa Francis unaosema kuwa mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni mwa changamoto  kubwa zinazomkabili mwanadamu na kuwa ni jambo la kimaadili linalohitaji mjadala toka pande zote za jamii. Taarifa zaidi na Joseph Msami.

(TAARIFA YA JOSEPH MSAMI)

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu ikiunga mkono matokeo ya waraka huo kuwa licha ya makubaliano ya kisayansi yanayoonyesha kuongezeka kwa joto katika mfumo mzima wa hali ya hewa lakini ni wazi kuwa kuongezeka kwa joto hilo hutokana ziadi na shughuli za kibinadamu.

Bwana Ban amesisitiza kuwa mwanadamu ana jukumu muhimu la kujali na kulinda sayari dunia ambayo ni nyumbani kwake na kuonyesha mshikamano kwa masikini na wale ambao ni waathirika wakuu wa madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Akizungumzia umuhimu wa tamko la kiongozi wa katoliki duniani Ban amesema.

(SAUTI BAN)

‘‘Sauti yake ya kimaadili ni sehemu ya kukuza wito wetu kwa watu wa imani zote, na sekta zote za jamii kuzungumzia kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.’’

Hata hivyo amezitolea wito serikali kulipa  kipaumbele suala mabadiliko ya tabia nchi na kupitisha makubaliano ya kimataifa katika mkutano mjini Paris Ufaransa mwaka huu huku pia akikaribisha mchango wa viongozi wa dini na watu wenye ushawishi katika jamii katika kushughulikai masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na kuimarisha maendeleo endelevu.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu wa shiriak la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni Irina Bokova, pamoja na mkuu wa shirika la UM la mazingira UNEP Achim Steiner wameunga mkono waraka huo.