Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuelekea siku ya watu wenye ulemavu wa ngozi, Kamishna Zeid azungumza

Kuelekea siku ya watu wenye ulemavu wa ngozi, Kamishna Zeid azungumza

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesema maadhimisho  ya kwanza kabisa ya siku ya kuhamasisha jamii kuhusu haki ya watu wenye ulemavu wa ngozi, Albino ni fursa ya kutambua vipaji adhimu walivyo navyo kundi hilo.

Siku hiyo itaadhimishwa tarehe 13 mwezi huu kwa kutambua umuhimu wa kulinda haki za watu wenye ulemavu wa ngozi wakati huu ambapo wanakumbwa na madhila ikiwemo kuuawa kwa imani za kishirikina.

Kamishna Zeid amesema ni lazima kutambua kuwa watoto wanaozaliwa na ulemavu wa ngozi, ni kutokana na jenetiki zilizopo kwenye familia zao lakini ukosefu wa uelewa huwatumbukiza kwenye madhila kutokana na rangi ya ngozi yao.

Ametaka serikali kuchukua hatua zaidi kuelimisha umma juu ya haki za albino na kuwapatia huduma bora za afya ikiwemo miwani ya jua na mafuta ya kuzuia uharibifu wa ngozi zao.