Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yasaidia wanafunzi wa Liberia baada ya Ebola

UNICEF yasaidia wanafunzi wa Liberia baada ya Ebola

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limeanza leo kusambaza vifaa 700,000 vya kusoma na kufundisha kwenye zaidi ya shuleni 4,400 nchini Liberia.

Msemaji wa UNICEF Christophe Boulierac amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, akieeleza kwamba lengo ni kusaidia wanafunzi kuendelea na elimu baada ya mlipuko wa Ebola.

Vifaa hivyo vitasambazwa kwa ushirikiano na serikali ya Liberia kwa kipindi cha wiki 12.

Bwana Boulierac ameongeza kwamba elimu ya zaidi ya watoto milioni moja iliathirika baada ya shule kufungwa kwa kipindi cha miezi sita.

Kwa mujibu wa UNICEF, shule zilipofunguliwa upya mwezi Februari mwaka huu, watoto laki nane wamerejelea shuleni, ikilinganishwa na idadi ya awali ya zaidi ya milioni moja kabla ya mlipuko huo.