UM watoa msaada wa kitaalamu kwa waathirika wa ubakaji DRC
Umoja wa Mataifa pamoja na washirika wake, umezindua kituo maalumu huko Kaskazini mwa Jamhuri ya Congo katika mji wa Bukavu kwa ajili ya kutoa mafunzo na mbinu rafiki kwa wahanga wa matukio ya ubakaji yaliyolikumba eneo hilo katika miezi ya hivi karibuni.
Mpango huo ambao umepewa jila la mji wa furaha, unaratibiwa kwa pamoja baina ya shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na watoto UNICEF na shirika moja lisilo la kiserikali lijulikanalo kama V-Day na imebainishwa kwamba kila mwaka wanawake 180 wenye umri wa miaka 14 hadi 35 watapatiwa mafunzo ya kitaalamu kabla ya kusambazwa kwenye maeneo ambayo yalikithiri kwa vitendo vya ubakaji hasa kwenye maeneo yaliyokumbwa na mizozo ya vita.
Kundi kubwa la wanawake wanaokadiriwa kufikia 200,000 walikumbana na vitendo vya kudhalilishwa kingono na kubakwa katika kipindi cha miaka 12 iliyopita. Mapema mwanzoni mwa mwaka huu visa vingine vya kuwepo kwa vitendo vya ubakaji viliripotiwa kufanyika katika eneo hilo la mashariki na kiasi cha watu 300 wengi wao wakiwa vijana na watu wazima walibakwa na makundi ya waasi na vikosi vya serikali.