Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulinzi wa amani wahitaji uungwaji mkono zaidi kimataifa- Ladsous

Ulinzi wa amani wahitaji uungwaji mkono zaidi kimataifa- Ladsous

Mkuu wa Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani katika Umoja wa Mataifa, Hervé Ladsous, amesema kwamba, wakati leo ikiadhimishwa Siku ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa, ukweli ni kwamba, mara nyingi walinda amani hao ndio tumaini pekee la maisha bora kwa raia ambao wamepewa mamlaka kuwahudumia.

Katika makala iliyochapishwa kwenye tovuti ya Huffington Post, Ladsous amesema, ili ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa uendelee kukabiliana ipasavyo na mizozo iliyopo sasa na siku zijazo, unahitaji kuungwa mkono kwa ubia wa kimataifa na utashi wa wote kusaidiana kuubeba mzigo na hatari.

Amesema katika baadhi ya maeneo ambako walinda amani wamepelekwa, hakuna amani ya kulinda. Ameongeza kuwa, katika baadhi ya mazingira magumu zaidi duniani, wahudumu wa Umoja wa Mataifa hulazimika kukumbana na hatari kila siku, katika muktadha wa misukosuko ya kisiasa na idadi kubwa ya watu wa kulinda, ambao aghalabu huwa wamejaa hofu.

Amesema, wakati huu wa kuwaenzi walinda amani 126 waliouawa mnamo mwaka 2014, vifaa bora vinahitajika ili kuwawezesha walinda amani kujilinda wenyewe na raia walio hatarini.