Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili vitendo vya kigaidi vinavyotishia amani na usalama

Baraza la Usalama lajadili vitendo vya kigaidi vinavyotishia amani na usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekuwa na mjadala kuhusu jinsi vitendo vya kigaidi vinavyotishia amani na usalama duniani, likimulika hasa tishio la wapiganaji wa kigaidi wa kigeni.

Akilihutubia Baraza hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema kuwa kusambaa kwa wapiganaji wa kigaidi wa kigeni, ambao wamejiunga na makundi ya kigaidi kama Da’esh na mengineyo, kumeongezeka duniani, tangu kupitishwa kwa azimio nambari 2178 la Baraza la Usalama

“Kumekuwa na ongezeko linalokadiriwa kuwa la asilimia 70, la wapiganaji wa kigaidi wa kigeni kote duniani, tangu kati ya mwaka 2014 na Machi mwaka 2015. Hali hii inaonyesha kuwa  wapiganaji hawa wengi, wanawapa magaidi rasilmali kubwa zaidi, na fedha kwa nchi wanakotoka, wakirudi huko.”

Ban amesema, hakuna nchi inayoweza kukabiliana na changamoto hii pekee, akiongeza kuwa nchi wanachama zinapaswa kuimarisha ushirikiano wao na ubadilishanaji habari, udhibiti wa mpiaka, na  kuimarisha mifumo ya sheria zao za uhalifu, kwa kuzingatia utawala wa sheria na viwango vya haki za binadamu

“Kuzingatia sheria ya kimataifa kikamilifu ni muhimu kwa ufanisi. Hili linajumuisha hususan sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, sheria ya wakimbizi na sheria ya kimataifa ya kibinadamu. Juhudi za kupambana na ugaidi zinapopuuza utawala wa sheria na kukiuka haki za msingi, zinaweza siyo kuwa kinyume na maadili zinazojaribu kutunza, bali pia kuchochea misimamo mikali katili.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Lithuania, Linas Antanas Linkevičius, ambaye nchi yake imekuwa ikishikilia kiti cha urais kwa mwezi huu wa Mei, amesema kuwa tishio la wapiganaji wa kigaidi wa kigeni ni sugu na linalobadilika badilika, ukizingatia hasa umri, jinsia na asili yao kijamii.

“Ni tishio linalotoa mtihani mkubwa kwa mbinu zilizopo za kupambana na ugaidi. Ingawa kuna mikakati ya kupambana na tishio hili, kuna mianya mikubwa ya utekelezaji, ikiwemo uwezo haba, rasilmali n ahata uelewa wa tatizo lenyewe.”

Amesema mbinu za kukabiliana na tishio hilo zinapaswa kubadilishwa ili kuzidi uwezo wa wapiganaji wa kigaidi wa kigeni, au angalau zilingane nao.