Skip to main content

Ustawi wa vijana wakabiliwa na changamoto lukuki : Alhendawi

Ustawi wa vijana wakabiliwa na changamoto lukuki : Alhendawi

Licha ya  juhudi za kuimarisha  ustawi wa vijana ambazo zimefanyika kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita bado kundi hilo linakabiliana na changamoto lukuki zikiwemo za kiuchumi na kijamii.

Ni kauli ya mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu vijana Ahmad Alhendawi ijumaa hii wakati wa mkutano wa baraza kuu la UM wa kuadhimisha miaka 20 ya mpango wa kimataifa wa usaidizi kwa vijana, maadhimisho ambayo  yamehudhuriwa na mawaziri, maafisa wa ngazi za juu wa UM na wawakilishi wa vijana kutoka nchi mbalimbali duniani.

Bwana Alhendawi amesema mpango huo uliopitishwa na baraza kuu miaka 20 iliyopita, ni hatua muhimu katika kutekeleza dira ya kusaidia maendeleo ya vijana na kuongeza kuwa mpango unataka upitishwaji wa sera za vijana kwa ngazi ya  kimataifa na kitaifa. Amesema kwa miongo miwili iliyopita kumekuwa na ongezeko kubwa la nchi kuidhinisha sera, sheria na mipango kwa ajili ya vijana.

Hata hivyo amesema mengi yanapaswa kufanywa akifafanua kuwa vijana wengi bado hawapati elimu bora, huduma za afya, na ushiriki katika siasa.

(SAUTI ALHENDAWI)

"Kimataifa kijana mmoja kati ya wanane hajaajiriwa, vijana 126 milioni hawawezi kusoma wala kuandika na wengine 63 milioni ambao ni vigori waliopaswa kuwa katika shule za sekondari hawajajiunga. Inakadiriwa kuwa pia vijana milioni 600 wanaishi katika maeneo yenye mizozo na kila dakika moja kijana wa kike anaathiriwa na virusi vya Ukimwi."

Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu vijana pia ameainisha kuwa zaidi ya vijana milioni 500 huishi chini ya kiwango cha dola mbili kwa siku.