Hali ya kiafya Yemen inazidi kuzorota:WHO

27 Mei 2015

Shirika la afya duniani, WHO limesema mzozo wa Yemen ukiingia wiki ya Kumi, idadi ya watu waliofariki dunia na majeruhi inazidi kuongezeka kila uchao huku raia wasio na hatia ndio wakiwa wahanga zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Margaret Chan katika taarifa iliyotolewa leo amenukuliwa akisema kuwa hadi sasa watu wapatao 2000 wameuawa huku 8000 wakiwa wamejeruhiwa wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.

Kama hiyo haitoshi zaidi ya watu Milioni Nane na Nusu wanahitaji huduma ya dharura ya matibabu ambapo amesema tayari WHO wamepeleka tani 48 za matibabu wakati wa siku tano za kusitisha mapigano lakini hiyo haitoshi.

Dkt. Chan amesema kitendo cha mzozo huo kuendelea na kuharibu miundombinu ya afya na kupoteza maisha ya raia hakipaswi kuachwa kiendelee hivyo ametaka pande zote husika kwenye mzozo huo kuzingatia wajibu wao kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu za kulinda raia na vituo vya afya sambamba na wahudumu wa afya.

Amesema hatua hiyo ni muhimu ili kuweza kufikisha haraka iwezekanavyo vifaa tiba pamoja na chanjo zinazohitajika ili kuokoa maisha ya watu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter