Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Diallo wa Guinea ateuliwa naibu mkuu wa MONUSCO

Diallo wa Guinea ateuliwa naibu mkuu wa MONUSCO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amemteua Mamadou Diallo wa Guinea kuwa Naibu mwakilishi wake maalum kwenye ujumbe wa kuweka utulivu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema Bwana Diallo anachukua nafasi ya Moustapha Soumaré wa Mali ambaye amekamilisha jukumu lake mwezi Machi mwaka huu.

Bwana Diallo atahudumu pia kama Mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa na mratibu wa masuala ya kibinadamu.

Katika taarifa hiyo Ban amemshukuru Bwana Soumaré kwa mchango wake wa kipekee wakati wa kipindi cha miaka mitatu kwa kusaidia utekelezaji wa mamlaka za MONUSCO na kuratibu shughuli za Umoja wa Mataifa nchini DRC.

Kabla ya kushika wadhifa huu mpya, Bwana Diallo amekuwa mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya ukimwi, UNAIDS kanda ya Afrika Magharibi na Kati.