Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaonya mdororo wa afya Yemen

WHO yaonya mdororo wa afya Yemen

Shirika la Afya Ulimwenguni(WHO) limeonya kuwa huduma za afya nchini Yemen nchi inayokumbwa na machafuko huenda zitakoma punde kutokana na ukosefu wa madawa, vifaa vingine muhimu na ukatakaji wa umeme mara kwa mara kunakoamabatana na ukosefu wa mafuta kwa ajili ya majenereta.

Mwakilishi wa WHO nchini Yemen, Dkt. Ahmed Shadoul amesema kuwa ukosefu wa mafuta umekatisha mara kwa mara ufanyaji kazi wa gari la kubebea wagonjwa wa dharura maarufu kama ambulance hatua ambayo pia imezuia ufikishwaji wa huduma za afya katika sehemu mbalimbali za nchi.

Kadhalika shirika hilo limetahadharisha kuwa mamilioni ya watoto  walio chini ya umri wa miaka mitano hawajapata chanjo dhidi ya surua kutokana na kukatika hovyo kwa umeme na ukosefu wa mafuta ya kuendesha jenereta zinazotumika kuendesha majokofu yanayohifadhi chanjo.

Kwa mujibu wa WHO hatua hiyo inaongeza hatari ya kuambukizana magonjwa kama vile surua ambayo imetamalaki nchini Yemen pamoja na polio ambayo ilitoweshwa lakini inaelekea kurejea upya.

Halikadhalika ukosefu wa maji safi umesababisha kuongeza hatari ya mlipuko wa ugonjwa wa kuhara na magonjwa mengine. Ripoti ya hivi karibuni ya ufuatiliaji magonjwa nchini Yemen imeonyesha kuongezeka maradufu kwa idadi ya visa vya magonjwa ya kuhara damu  kwa watoto walioko katika umri wa chini ya miaka mitano pamoja na surua huku malaria ikitajwa kunyemelea.

Pia utafiti umeonyesha kiwango kikubwa cha utapiamlo kwa wanawake na wanaume na watoto walioko chini ya umri wa miaka mitano.