Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lataka waasi nchini Mali wasaini makubaliano ya amani

Baraza la Usalama lataka waasi nchini Mali wasaini makubaliano ya amani

Wajumbe wa Baraza la Usalama wamevisihi vikundi vilivyojihami kusaini makubaliano ya amani na maridhiano nchini Mali yaliyosainiwa Machi tarehe 1 na wawakilishi wa serikali, umoja wa mitandao ya vikundi vilivyojihami na timu ya kimataifa ya mazungumzo.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, kufuatia mazungumzo maalum yaliyofanyika tarehe 9, Aprili, kwenye Baraza la Usalama.

Wamesema makubaliano hayo ni hatua ya msingi katika kufikia amani ya kudumu nchini humo, wanachama wa Baraza la Usalama wameongeza kwamba ni wajibu wa wadau wote waliopo Mali kuhakikisha yaliyokubaliwa yanatekelezwa.

Aidha wanachama wa Baraza hilo wamesisitiza umuhimu wa kuunda mifumo ya kufuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo ya amani, wakisema mfumo huu unapaswa kuongozwa na Mali.

Hatimaye wameelezea wasiwasi wao kuhusu kuzorota kwa hali ya usalama kaskazini mwa nchi na kuongezeka kwa idadi ya mashambulizi, ikiwemo dhidi ya MINUSMA, wakikariri wito wao kwa pande zote za mzozo kujizuia kufanya vitendo vinavyohatarisha mwelekeo wa amani.