Ban aitaka Nigeria kufanya uchaguzi wa magavana kwa amani

Ban aitaka Nigeria kufanya uchaguzi wa magavana kwa amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezungumzia uchaguzi wa magavana na wabunge nchini Nigeria hapo kesho April 11, na kulitaka taifa hilo kuendesha uchaguzi huo kwa amani na utulivu.

Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya msemaji wa Katibu Mkuu, Bwana Ban ana matumaini kuwa amani itatawala kama ilivyokuwa katika uchauguzi wa awali mnamo March 29 ambapo Nigeria ilifanya uchaguzi wa Rais na wabunge .

Amesema utaifa ulioonyeshwa na viongozi wa kisiasa umeweka hatua muhimu katika mchakato wa demokrasia ya taifa hilo la Magharibi mwa Afrika.

Bwana Ban amewataka wadau wa siasa nchini Nigeria kuendelea kutimiza ahadi zao chini ya mkataba wa Abuja na kujizuia dhidi ya matamko ya kulaani na kuchochea ambayo husababisha machafuko.