Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yatarajia kupeleka misaada kwa watu 162,000 Vanuatu

WFP yatarajia kupeleka misaada kwa watu 162,000 Vanuatu

Shirika la mpango Chakula Duniani WFP linasaidia serikali ya Vanuatu katika jitihada zake za kuwapelekea watu 162,000 vyakula vya dharura vikiwemo mchele, maharage na biskuti baada ya kimbunga PAM kupinga nchi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva, msemaji wa WFP Elisabeth Byrs amesema wataaalam wa WFP waliofika Vanuatu saa 48 tu baada ya tukio la kimbunga bado wanaendelea kushirikiana na serikali ili kubaini mahitaji ya walioathirika.

Hata hivyo msemaji huyo wa WFP amesema ni vigumu sana kujua hali halisi kwani Vanuatu ina jumla ya visiwa vidogo 81 ambavyo vimesambaa kwenye eneo la kilomita 13,000 za mraba kwenye bahari ya Pacifiki.

« Ni vigumu sana kujua ni kwa kiasi gani akiba za chakula zimeharibika kwenye visiwa hivi. Tunatumai kwamba raia wameweza kuokoa baadhi ya akiba. Lakini kwa sasa hivi tuko na matatizo ya usafirishaji, hasa kati ya visiwa vidogo, na foleni kwenye uwanja wa ndege »

WFP imesema itapeleka wataalam wa usafirishaji ili kuisaidia serikali katika usambazaji wa misaada na pia vifaa vya mawasiliano ili kuwasaidia wahudumu wa kibinadamu.