Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misitu hudhibiti mabadiliko ya tabianchi: FAO

Misitu hudhibiti mabadiliko ya tabianchi: FAO

Misitu ina jukumu la msingi katika kupunguza kiwango cha hewa ya ukaa angani na hivyo kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.

Ni ujumbe wa José Graziano da Silva, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo FAO, aliotoa leo katika maadhimisho ya siku ya misitu duniani.

Hata hivyo, amesisitiza kwamba misitu huathirika na mabadiliko ya tabianchi.

“ Bila misitu, upatikanaji wa maji uko hatarini. Bila misitu na miti, maeneo ya pwani, milimani na mashambani yako hatarini zaidi kukumbwa na majanga. Kwa hiyo, misitu ni muhimu kwa usalama wa chakula, kwa sasa na kwa maisha ya baadaye. Pia misitu ni muhimu kwa uwiano wa kiwango cha hewa ya ukaa duniani.”

Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO ameeleza kwamba uharibifu wa misitu huongeza kiwango cha hewa ya ukaa angani na kwa upande mwingine, ukuaji wa misitu unavuta hewa hiyo inayosababisha ongezeko la halijoto duniani.

Amesema wakati wa kuandaa malengo endelevu ya maendeleo, ni muhimu kuunda mfumo endelevu wa kutumia rasilimali za misitu, kupitia upandaji wa miti na kudhibiti ukataji miti.

Kwa mujibu wa FAO, misitu imetandaa kwenye theluthi moja ya ardhi iliyopo ulimwenguni, ikiwapatia hifadhi asilimia 80 ya bayoanuai na pia ni chanzo cha riziki kwa watu bilioni 2.4 duniani.