Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wakimbia Sudan kutafuta hifadhi Sudan Kusini

Watu wakimbia Sudan kutafuta hifadhi Sudan Kusini

Nchini Sudan Kusini, idadi ya wakimbizi wanaokimbia mapigano yanayoendelea nchini Sudan imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 100 tangu mwezi mmoja uliopita.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi, UNHCR, zaidi ya wakimbizi 3,000 wamekimbia majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile ili kutafuta hifadhi katika kambi za wakimbizi zilizopo nchini Sudan Kusini, katika jimbo la Unity, karibu na mpaka wa Sudan.

William Spindler, msemaji wa UNHCR amesema tayari kambi hizo zimejaa, hali ya wakimbizi ikiwa tete.

“ Wakimbizi wamewaambia wafanyakazi wa UNHCR kwamba wamekimbia mapigano na uhalifu unaoendelea katika maeneo ya milima ya Nuba, yakiwemo mabomu yanayorushwa kutoka angani na mashambulizi kadhaa. Wakimbizi wameelezea pia ukosefu wa kazi na elimu katika maeneo yao kama sababu za kukimbia. Wengi wao wanafika kwa malori, wengine wakifika kwa miguu. Asilimia 70 ni watoto, tukikadiria kwamba miongoni mwao asilimia 10 wameathirika na utapiamlo na ugonjwa wa surua”

Aidha Spindler anaeleza kwamba UNHCR inatarajia kupokea wakimbizi zaidi katika wiki zijazo, huku tayari watu mia 500 wakiingia nchini Sudan Kusini kila wiki, na kambi ya Yida ikiwa imepokea wakimbizi zaidi ya 80,000.