Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakutana kuhusu hali nchini Burundi

Baraza la Usalama lakutana kuhusu hali nchini Burundi

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limefanya mkutano kujadili hali nchini Burundi, na kufanya pia mashauriano kuhusu Ofisi ya Umoja wa Mataifa Burundi, BNUB.Wakati wa mkutano wa leo, Baraza la Usalama limehutubiwa na Mkuu wa Masuala ya Kisiasa katika Umoja wa Mataifa, Jeffrey Feltman, ambaye amewasilisha ripoti ya mwisho ya Katibu Mkuu kuhusu Ofisi ya Umoja wa Mataifa Burundi, BNUB, ambayo ilikamilisha majukumu yake na kufungwa mnamo Disemba mwaka jana.Bwana Feltman amesema Burundi imepiga hatua za kina na kumudu kukabiliana na changamoto sugu tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

“Burundi iliweka mfumo wa kugawana mamlaka, ikaweka taasisi zenye usawa kikabila, ikfanya uchaguzi wa mara kwa mara, na bado inazingatia ahadi ya maridhiano ya kitaifa. Burundi ni salama zaidi kuliko ilivyokuwa muongo mmoja uliopita.”

Hata hivyo, Bwana Feltman amesema moyo wa Arusha na kanuni zake za mashauriano, maafikiano na demokrasia umemomonyoka, tangu uchaguzi wa mwaka 2010

“Chuki za kisiasa zinaendelea kuzuia juhudi za kuimarisha amani, demokrasia na maendeleo. Bado kuna wasiwasi kuhusu kutoweka uhuru wa kisiasa, vizuizi kwa haki ya kufanya mikutano na kujieleza, na changamoto za kujenga mfumo huru wa sheria, ambao ni muhimu kwa demokrasia.”