Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaelezea wasiwasi kuhusu kurejeshwa kwa wakimbizi Nigeria

UNHCR yaelezea wasiwasi kuhusu kurejeshwa kwa wakimbizi Nigeria

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, limeeleza kutiwa wasiwasi na kurejea kwa mamia ya wakimbizi Nigeria katika operesheni ya pamoja iliyopangwa na Gavana wa jimbo la Borno na mamlaka za Niger, kuanzia Januari 14 mwaka huu, na kutaka operesheni hiyo isitishwe. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

UNHCR imesema inatiwa wasiwasi na jinsi wakimbizi hao wanavyorejeshwa, ikizingatiwa kuwa hali ni tete katika jimbo la Borno, kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni. Kwa mantiki hiyo, imeomba mamlaka za Nigeria na Niger kusitisha operesheni hiyo hadi pale utakapowekwa utaratibu mwafaka wa ulinzi na sheria, baina ya Nigeria, Niger na UNHCR.

Kwa mujibu wa UNHCR, wakimbizi wanaokimbia machafuko kaskazini mashariki mwa Nigeria wanaendelea kuwasili Niger na Chad, wakitoa habari za kuhuzunisha za mauaji na uharibifu. William Spindler ni msemaji wa UNHCR

“Timu zetu zimesema kuwa wakimbizi wanaelezea ukatili mkubwa waliokumbana nao au walioshuhudia wakati wa mashambulizi kwenye mji wa Baga tarehe 3 na tarehe 7 Januari. Mwanamke mmoja aliyekimbia na wanawe watano na mumewe amesema aliona waasi wakiwagonga watoto kwa magari, kuwapiga watu risasi na kutumia visu kukata mashing ya wengine mitaani.“

Kulingana na UNHCR, mabasi mengine 11 yameegeshwa matika mji wa Gagamari kwenye jimbo la Diffa, Niger, yakisubiri kuwarejesha wakimbizi wengine Nigeria.