Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kaimu Mkuu wa UNAMID azuru Darfur Magharibi

Kaimu Mkuu wa UNAMID azuru Darfur Magharibi

Kaimu Mwakilishi maalum wa pamoja wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa huko Darfur nchini Sudan, Abiodun Bashua amekuwa na ziara ya siku mbili magharibi eneo hilo kutathmini hali ya usalama na ushirikiano baina ya ujumbe anaoongoza na wakazi wa maeneo hayo.

Mathalani alikuwa na mazungumzo na Gavana wa jimbo la Darfur Magharibi Haider Galikoma Ateem ambapo alimwelezea hali ya sasa na ushiriki wa serikali wa kuwapatia huduma za msingi wananchi wanaorejea makwao.

Halikadhalika wamejadili ushirikiano kati ya serikali ya Sudan na ujumbe pamoja wa AU na Umoja wa Mataifa, UNAMID hususan maendeleo ya kutekeleza hatua za mwisho za usalama kwa kikundi cha Liberation and Justice Movement, LJM.

Bwana Bashua amesisitiza kuwa UNAMID imeazimia na itasaidia mipango ya usalama kwa vikosi vya LJM kama hatua muhimu ya kuleta amani ya kudumu Darfur.

Kaimu Mkuu huyo wa UNAMID pia amesisitiza kuwa ujumbe huo utaendelea kuwapatia usaidizi wananchi wa Darfur Magharibi kupitia miradi ya ziada ya maendeleo hususan ile inayoleta huduma za maji safi na salama kwenye kambi za wakimbizi wa ndani.