Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani 8 wajeruhiwa katika shambulio la kigaidi Mali

Walinda amani 8 wajeruhiwa katika shambulio la kigaidi Mali

Shambulio la kigaidi dhidi ya msafara wa wanalinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Matiafa nchini Mali, MINUSMA, kwenye maeneo ya Gao hapo jana limesababisha  kujeruhiwa kwa walinda amani 8.

Kwa mujibu wa MINUSMA, wanajeshi hao walikuwa wanarudi kutoka likizo nchini mwao, Niger, na ndipo gari yao ilipolipuliwa na bomu. Miongoni mwa majeruhi hao, watatu wako kwenye hali mbaya na  wamesafirishwa Dakar, Senegal, kwa matibabu.

MINUSMA imelaani vikali shambulizi hilo na kuwaomba wadau wote wanaoshirikiana katika utaratibu wa amani kujitahidi kuzuia vitendo kama hivyo na kuhakikisha watekelezaji wanapelekwa mbele ya sheria.

Akizungumza na redio ya Umoja wa Mataifa, Radhia Achouri, ambaye ni mkuu wa mawasiliano wa MINUSMA, amesema wanashuku kuwa watekelezaji wa shambulio hilo ni kundi la waasi kutoka kaskazini mwa Mali, ambalo limeshawahi kulenga MINUSMA na wanajeshi wa Mali.

Kwa kweli tumejitahidi sana ili kuboresha jinsi tunavyofanya kazi, ili kuhakikisha kwamba tunaweza kuingilia kati wakati wowote panapohitajika ili kulinda raia wa Mali. Lakini aina hii ya shambulio haiwezi kuzuiliwa, eneo tunapofanya kazi ni kubwa sana, na sisi hatupo wengi sana. Tunatumia nyenzo zote ili kuhakikisha kwamba wanajeshi wetu hawaathiriki na ugaidi kama huo na kusaidia Mali na raia wa Mali ili kuleta utulivu na usalama nchini humo”