Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi Sudan Kusini wachukue hatua kukomesha Mateso: UM

Viongozi Sudan Kusini wachukue hatua kukomesha Mateso: UM

Viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa wamesema miaka mitatu baada ya Sudan Kusini kujitenga kutoka Sudan, bado taifa hilo linakabiliwa na migogoro ambayo imetowesha ndoto za wengi na kutishia mustakhbali wa taifa hilo changa.

Katika tahariri waliyochapisha leo kwa pamoja kwenye tovuti ya Huffington Post ya Marekani, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono kwenye mizozo, Zainab Hawa Bangura, Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari Adama Dieng , Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu anayehusika na wajibu wa kulinda raia na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu watoto na migogoro ya silaha, Leila Zerrougui, wamesema mapigano katika taifa hilo yameathiri raia hususan wanawake na watoto.

Viongozi hao wamesema pande zote katika mgogoro zimetekeleza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria ya kibinadamu ya kimataifa, ikiwa ni pamoja mauaji yasiyo halali, kupotea kwa watu na unyanyasaji wa kijinsia.

Wakati mwingine ukiukaji huu walisema unaweza kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huku raia wakilengwa kwa makusudi kwa mising ya kikabila na msimamo wao wa kisiasa.

Halikadhalika, washauri hao wamesema tangu kuzuka kwa mapigano mwezi Disemba mwaka jana zaidi ya watu 10,000 wameuawa, watu 1.9 kufurushwa makwao huku mamilioni ya watu wakikumbwa na uhaba wa chakula.