Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wengine wauawa Yemen, UNICEF yatoa tamko

Watoto wana haki ya kupata elimu. (Picha ya OCHA - Yemen)

Watoto wengine wauawa Yemen, UNICEF yatoa tamko

Nchini Yemen shambulio la bomu kwenye gari limesababisha vifo vya watoto wapatao 15 ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limelaani vikali, likisema tukio hilo na lile lingine huko Pakistani yamemalizia vibaya mwaka uliogubika shari kwa watoto duniani kote.

Taarifa ya UNICEF imesema hakuna jambo lolote linaloweza kuhalalisha ukatili huo dhidi ya watoto wanapokuwa wanakwenda kusaka elimu au kwa walimu wanaojituma kuelimisha watoto hao.

UNICEF imesema uhai wowote uliopotezwa leo huko Peshawar Paksitan au Al Badya Yemen ni ishara ya kupotezwa kwa mustakhbali wa eneo husika.

Mwaka huu umegubikwa na mashambulizi dhidi ya shule, wanafunzi na walimu ambapo UNICEF imesema ni kwa mantiki hiyo inataka mwaka 2015 uwe wa kupatia kipaumbele ulinzi wa watoto dhidi ya aina zozote za ukatili iwe kwenye mizozo au kwenye amani, shuleni au majumbani.