Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ikiendelea hivi Sudan Kusini tutachukua hatua thabiti: Baraza la Usalama

UN Photo.
baraza-la-usalama

Hali ikiendelea hivi Sudan Kusini tutachukua hatua thabiti: Baraza la Usalama

Ikiwa leo ni mwaka mmoja tangu kuanza kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limerejelea tena nia yake ya kuanza kufikiria uwezekano wa kuchukua hatua thabiti dhidi ya wanaokwamisha mchakato wa amani nchini  humo.

Taarifa hiyo ya Rais wa Baraza imeungwa mkono na wajumbe ambapo inasema matarajio ya amani waliyokuwa nayo wananchi wa Sudan Kusini mwaka 2011  yametumbukia nyongo na sasa mapigano yaliyoanza mwaka mmoja uliopita umezidisha machungu zaidi.

Baraza pamoja na kutambua hatua zinazoendelea kuchukuliwa kikanda na kimataifa kumaliza mzozo wa Sudan Kusini, limesema litashauriana na pande mbali mbali kufikiria hatua hizo thabiti ikiwemo vikwazo vinavyolenga wanaokwamisha mpango wa amani.

Hata hivyo wameelezea shukrani zao kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS wa kulinda makumi ya maelfu ya raia huku wakikumbuka walinda amani waliopoteza maisha wakitekeleza jukumu la Umoja huo la kulinda amani.

Wametaka Rais Salva Kiir Mayardit, Makamu wake wa zamani Riek Machar Teny na pande zote kujizuia na ghasia na badala yake kutekeleza mkataba wa kumaliza mzozo huo uliotiwa saini tarehe Tisa Mei.