Washindi wa tuzo ni kiashiria hatua zinaweza kuchukuliwa: Ban

11 Disemba 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki-moon amezungumza kwenye tukio la kutoa tuzo kwa wabunifu wa mbinu za kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi huko Lima, Peru na kusema washindi hao ni kiashiria kuwa kuna uwezekano wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Taarifa zaidi na Abdullahi Boru.(Taarifa ya Abdullahi)

Ban amesema taarifa ya jopo la wataalamu iliyotolewa mwezi uliopita imeweka bayana kuendelea kwa shughuli za binadamu zitakazokwamisha udhibiti wa kiwango cha joto duniani chini ya nyuzi joto mbili ya kipimo cha selsiyasi.

Hata hivyo amesema washindi wa tuzo hizo ni habari njema kwamba kuna njia na ufumbuzi wa kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema washindi hao ni kiashiria cha nafasi ya wanawake kwenye kudhibiti mabadiliko ya tabianchi na kwamba washindi hao wanaboresha maisha ya wakazi maskini mijini na kuibuka na mbinu rahisi za udhibiti.

Ban amesema ni matumaini yake ubunifu wa washindi hao utaweka hamasa kwa viongozi wanapotunga sera ili hatimaye kufikia makubaliano ya pamoja ya mazingira mwakani huko Paris

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter