Baraza la usalama lajadili magaidi kuteka nyara na kudai fidia

24 Novemba 2014

Harakati za kukabiliana na vitendo vya magaidi kuteka nyara watu na kudai fidia ni lazima ziende sambamba na hatua za kuzuia vitendo hivyo, amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Kurugenzi ya kamati ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na ugaidi, CTED Jean-Paul Laborde. Taarifa kamili na Abdullahi Boru.

(Taarifa ya Abdullahi)

Bwana Laborde amesema hayo kwenye kikao cha kamati hiyo kilichokutana kujadili tabia ya vikundi vya magaidi kuteka watu nyara na kudai fidia ambapo ilielezwa kuwa vitendo hivyo pamoja na kulenga kuibua madai ya kisiasa pia ni mbinu ya vikundi hivyo kupata fedha za kujiendesha.

Mkurugenzi huyo amesema harakati sahihi za kuokoa mateka zinaweza kuzaa matunda lakini zinaweza kuwa na madhara..

(Sauti ya Laborde)

“Vinaweza pia kuathiri usalama na taswira ya mateka. Hofu hii ni kitovu cha hatua zitakazozingatiwa wakati wa mipango ya kusaka kuachiwa huru kwa mateka ikiwemo kupitia njia za kidiplomasia au kijeshi.”

Hata hivyo amesema hatua za kukabili vitendo hivyo zienda sambamba na kuvizuia.

(sauti ya Laborde)

“Na mafanikio ya yanategema ushirikiano wa pamoja na wa karibu baina ya pande zote na hii inajumuisha siyo tu mashirika ya kiserikali tu na ya kimataifa bali pia vyombo vya habari na sekta binafsi  hususan mashirika ya bima yaliyojikita kwenye ulipaji hizo fidia kwenye maeneo husika.”

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter