Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mdudu anayeharibu matunda ni yule yule, lakini aina tofauti- FAO

Picha ya FAO/USDA/Scot Bauer

Mdudu anayeharibu matunda ni yule yule, lakini aina tofauti- FAO

Imebainika kuwa aina nne za wadudu waharibifu mno katika kilimo ni wenye asili moja, kulingana na matokeo ya utafiti wa kimataifa yaliyochapishwa leo na Shirika la Chakula na Kilimo, FAO.

Kwa mujibu wa wataalam wa FAO, ugunduzi huu utasaidia kupunguza baadhi ya vikwazo vya biashara kimataifa, na pia kusaidia juhudi za kukomesha uwezo wa wadudu hao waharibifu kuzaliana.

Kwa mujibu wa utafiti huo, wadudu wajulikanao kama wadudu wa tunda la papai wa nchi za bara Asia na Ufilipino, wana asili moja iitwayo  kisayansi, Bactrocera dorsalis, na wamekuwa wakisababisha uharibifu mkubwa kwa kilimo cha bustani na usalama wa chakula bara Asia, Afrika, Pasifiki na maeneo ya Amerika ya Kusini.

Uwezo wa kutambua aina za wadudu waharibifu ni muhimu katika kudhibiti wadudu hao, na pia kuongoza hatua za karantini au upigaji marufuku dhidi ya bidhaa za chakula au kilimo zinazouzwa ng’ambo, kama vile matunda na mboga mboga.