Licha ya shule kufungwa, watoto kuendelea kupata masomo: UNICEF

22 Oktoba 2014

Nchini Sierra Leone, baada ya mlipuko wa Ebola kusababisha kufungwa kwa shule zote ili kudhibiti maambukizi, serikali imeanzisha matangazo ya vipindi vya elimu kupitia radio.

Matangazo hayo yamewezekana kupitia usaidizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF ambalo limesema ni hatua muhimu ili watoto waendelee kupata haki yao ya msingi ya elimu.

Afisa wa elimu wa UNICEF nchini Sierra Leone Uche Ezirim amesema mpango huo umezinduliwa wiki hii kupitia radio ya Taifa na lengo ni kufikia zaidi ya watoto Milioni Moja na Nusu.

Masomo ni pamoja na kiingereza, hisabati, fizikia, elimu ya kijamii pamoja na afya inayogusia pia ugonjwa wa Ebola.

Matangazo hayo kupitia radio ya Taifa ya Sierra Leone yanahusisha pia mitandao 41 ya radio nchini kote inayoratibiwa na chama cha waandishi wa habari na mtandao huru wa radio.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter