Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa MONUSCO ampa heko Dr. Mukwege kwa kazi yake DRC

Daktari Denis Mukwege wa DRC.(Picha ya Radio Okapi maktaba)

Mkuu wa MONUSCO ampa heko Dr. Mukwege kwa kazi yake DRC

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, MONUSCO, Martic Kobler, amekaribisha tuzo iliyotolewa kwa Daktari Denis Mukwege wa DRC, akisema kwamba tuzo hiyo inasaidia kumulika mapambano yake yasiyoonyesha kuchoka, anapojaribu kuutokomeza ukatili wa kingono dhidi ya wanawake, watoto na wanaume nchini DRC.

Hospitali ya Panzi katika Jimbo la Kivu ya Kusini, ambayo ilianzishwa na Dkt. Mukwege na ambayo imehudumu kwa miaka 15, inajulikana kote duniani kwa huduma zake kwa waathiriwa wa ukatili wa kingono.

Bwana Kobler amesema tuzo hiyo inatoa heshima kwa kazi kubwa ya mtu ambaye kwa takriban kipindi cha mwongo mmoja, amekuwa akijitoa katika mapambano hayo.

Ameongeza kuwa tuzo hiyo pia inaonyesha uzingativu wa jamii ya kimataifa katika kuunga mkono amani na usalama katika DRC. Amesema tuzo hiyo pia ni ujumbe kwa makundi yote yenye silaha na watu wanaoendelea kutenda ukatili dhidi ya raia wa Kongo, kwamba ukatili huo unapaswa kukomeshwa.