Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna uhusiano kati ya maendeleo endelevu na usawa wa jinsia- UN Women

Wanawake kutoka Rwanda wanasherehekea baada ya kumaliza mafunzo ya kilimo(Picha:Stephanie Oula/UN Women)

Kuna uhusiano kati ya maendeleo endelevu na usawa wa jinsia- UN Women

Shirika linalohusika na masuala ya Wanawake katika Umoja wa Mataifa, UN Women, limetoa ripoti mpya kuhusu utafiti wa kimataifa kuhusu mchango wa wanawake katika maendeleo, wakati dunia ikijiandaa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Umaskini, ambayo ni Oktoba 17.

Ripoti hiyo ambayo inaweka wazi hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuleta mabadiliko, imesema pia kuwa maendeleo ya kina endelelevu hayawezi kufikiwa bila kuzingatia usawa wa jinsia, haki za wanawake na kuwawezesha.

Ripoti pia imebaini kuwa kuna haja ya kubadili sera ili kuangazia haki za wanawake, uwezo wao, mchango wao katika uongozi na kazi wanazozifanya bila kulipwa. Inatoa pia tathmini ya kina kuhusu masuala ya maendeleo endelevu, changamoto zilizopo na masuluhu yake kwa mtazamo wa jinsia.

Ripoti hiyo pia imesema kuwa mabadiliko ya tabianchi yana athari kubwa kijamii, kiuchumi na kimazingira, na kwamba athari zake hizo zinadhihirika katika mafuriko, ukame, na uharibifu wa ardhi na vitega riziki.