Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Luxembourg yaongeza mchango wake kwa Mfuko wa Dunia wa Malaria, HIV na TB

Nembo ya global fund.(maktaba)

Luxembourg yaongeza mchango wake kwa Mfuko wa Dunia wa Malaria, HIV na TB

Taifa la Luxembourg limetangaza kuwa linaongeza mchango wake wa fedha kwa Mfuko wa Dunia unaofadhili vita dhidi ya malaria, HIV na kifua kikuu mwaka 2014, huku Marekani na Uingereza pia zikiongeza ufadhili wao.

Waziri Mkuu wa Luxembourg, Xavier Bettel, alitangaza hayo mnamo Jumamosi kwenye tamasha la Raia wa Dunia (Global Citizen) lilifanyika mjini New York, akisema kuwa serikali yake itachangia Euro    500,000 zaidi kwa mwaka 2014, ikiwa ni nyongeza kwa Euro milioni 2.5 za awali.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Global Fund, Mark Dybul, amewasifu watu wa Luxembourg kwa kuonyesha ukarimu wao katika kuunga mkono juhudi za Mfuko wa Dunia kushirikiana na wadau ili kutokomeza HIV, Kifua kikuu na malaria. Ameongeza kuwa sayansi imedhihirisha kuwa kuna ujuzi wa kuyatokomeza magonjwa hayo, ikiwa kutakuwa na uwekezaji mkubwa katika juhudi za kupambana nayo.