Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nina wasiwasi na mustakhbali wa watoto ukanda wa Gaza: Mtaalamu maalum

UN Photo/Violaine Martin
Makarim Wibisono.

Nina wasiwasi na mustakhbali wa watoto ukanda wa Gaza: Mtaalamu maalum

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu kwenye maeneo ya Palestina yanayoshikiliwa tangu mwaka 1967, Makarim Wibisono ameelezea wasiwasi wake juu ya madhara yanayokumba raia hususan watoto kwenye Ukanda wa Gaza kufuatia operesheni za kijeshi zilizofanywa na Israel kwa siku 50 kuanzia Julai Saba mwaka huu.

Katika taarifa yake baada ya ziara yake kwenye eneo hilo, Wibisono amesema madhara ya operesheni hiyo iliyoacha maelfu wamefariki dunia na wengine vilema, ni pamoja na makumi ya maelfu ya watoto kukumbwa na majinamizi kwa kile walichoshuhudia wakati wa mashambulizi hayo.

Mathalani amesema watoto walishuhudia wanafamilia wao wakiuawa na kitendo hicho kinaibua maswali juu ya uwezekano wa ukiukwaji wa sheria za kibinadamu na haki za binadamu.

Bwana Wibisono amesema kwenye eneo ambalo nusu ya watu wake Milioni Moja nukta Nane wana umri wa chini ya miaka 18, ni janga kubwa litakalothibitika baadaye kwani hao ndio walioshuhudia madhila hayo ya siku 50.

Kutokana na hali hiyo, watoto wanashindwa kulala, wanashindwa kula chakula na tabia nyingine ambazo amesema ziko dhahiri shuleni.

Mtaalamu huyo ameisihi Israel kuzingatia misingi ya matumizi ya silaha za moto akisema kuwa kati ya tarehe 12 Juni hadi 31 Agosti mwaka huu zaidi ya wapalestina 27 waliuawa akiwemo mtoto mwenye umri wa miaka 11.

Ripoti na mapendekezo ya Bwana Wibisono itawasilisha kwenye mkutano wa Baraza la haki za binadamu mwezi Machi mwakani.