Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Somalia walioko Kenya kurejea nyumbani kwa utaratibu unaofaa: Rais Mohamoud

UN Photo/Kim Haughton
Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamoud.

Wakimbizi wa Somalia walioko Kenya kurejea nyumbani kwa utaratibu unaofaa: Rais Mohamoud

Somalia ikishirikiana na Kenya na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, ina mpango wa kuwarejesha nyumbani kwa maridhiano wakimbizi wa Somalia wanaoishi nchini Kenya.

Hiyo ni kauli ya Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamoud aliyotoa akizungumza na Radio ya Umoja wa Mataifa kando mwa hotuba yake ya kwenye mjadala mkuu wa kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Rais Mohamoud amesema wakimbizi wa Somalia walio Kenya wamekuwa huko kwa muda mrefu, na wengine wao wameishi Kenya kuliko walivyoishi Somalia, na hivyo ni heri kuwarejesha nyumbani kwa kufuata utaratibu mzuri.

(Sauti ya Hassan Sheikh)

Kwa hiyo, kazi inaendelea, japo bila shaka itachukua muda. Cha msingi ni kwamba, sisi kama serikali ya Somalia tutawapokea wale wakimbizi wa Somalia wanaoishi katika kambi za wakimbizi nchini Kenya. Na serikali ya Kenya imekubali kushirikiana na serikali ya Somalia na Umoja wa Mataifa kuwarejesha wakimbizi hao makwao kwa njia laini na utaratibu ufao”

Akizungumzia ugonjwa wa Ebola, Rais huyo amesema licha ya kwamba kisa cha ugonjwa huo hakijaripotiwa nchini humo, serikali yake imekubaliana na Muungano wa Afrika kwamba wanajeshi wa kulinda amani wanaotoka mataifa ya Magharibi mwa Afrika wasiruhusiwe kwenda makwao.

(Sauti ya Hassan Sheikh )

Nchini Somalia tuko na vikosi vya kulinda amani kutoka baadhi ya nchi zilizoathirika, na kwa kawaida, utaratibu ni vikosi hivyo huwa vinabadilishwa baada ya muda, kikosi kimoja kinaondoka na kingine kinakuja. Sisi tumekubaliana na Muungano wa Afrika na vikosi vilivyoko Somalia kwamba wasibadilishwe na ombi letu limekubaliwa."