Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola imedhibitiwa Nigeria: Rais Jonathan

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria.Picha:UN/Cia Pak

Ebola imedhibitiwa Nigeria: Rais Jonathan

Wakuu wa nchi na serikali wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wamejulishwa kuwa mlipuko wa Ebola huko Nigeria umedhibitiwa na lakini hali bado si shwari huko Sierra Leone na Liberia na hivyo ni vyema hatua zikachukuliwa kwani Ebola inatishia mustakhbali wa nchi hizo.

Taarifa hizo zimetolewa na Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria katika hotuba yake kwenye mjadala mkuu wa baraza hilo siku ya Jumatano wakati huu ambapo Ebola imesababisha vifo vya watu zaidi ya 2500 huko Sierra Leone, Guinea, Liberia na Nigeria.

(Sauti ya Rais Jonathan)

"Kupitia jitihada za pamoja za wataalamu wetu wa afya,shirika la afya duniani na wadau wa kimataifa tumeweza kudhibiti kirusi cha Ebola na tunaweza kusema kwa kujiamini kuwa hii leo Nigeria hakuna Ebola.”

Rais Jonathan amesema wanaendelea kuunga mkono jitihada za kudhibiti Ebola Guinea, Liberia na Sierra Leone ikiwemo kutoa mafunzo kwa watoa huduma.

Amesema ni vyema jamii ya kimataifa kuchukua hatua sahihi kudhibiti ugonjwa huo badala ya kuamua kuzitenga nchi zenye mlipuko kwa kusitisha safari za ndege na hata biashara.