Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lasisitiza umuhimu wa kufuatilia viikwazo dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran

Wajumbe wa Baraza la Usalama.(Picha UM//Paulo Filgueiras)

Baraza la Usalama lasisitiza umuhimu wa kufuatilia viikwazo dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran

Baraza la Usalama limekutana Jumatatu tarehe 15 Septemba, kwa ajili ya kupitia ripoti ya kamati kuhusu azimio namba 1737 linalolenga kudhibiti mpango wa nyuklia wa Iran. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mwakilishi wa Kudumu wa Australia, Balozi Gary Quiland, amesema kwamba kamati hiyo imeendelea kufuatilia utekelezaji wa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya mpango huo, akiziomba nchi wanachama kupeleka ripoti zao za kitaifa mbele ya kamati ili kuhakikisha ufanisi wa vikwazo hivyo.

Balozi huyo ameeleza kwamba kamati imeiandikia Iran kuhusu meli ya silaha za kawaida iliyosimamishwa katika Bahari ya Shamu, mwezi Machi mwaka huu, ili kuiomba maelezo zaidi, lakini Iran mpaka sasa hivi haijajibu kitu chochote.

Kamati ya vikwazo kuhusu azimio 1737 la Baraza la Usalama ina jukumu la kufuatilia vikwazo dhidi ya uzuiaji wa uenezaji wa silaha za kinyuklia na Iran. Kamati hiyo huripoti mbele ya Baraza la Usalama kila miezi mitatu.