Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu laadhimisha siku ya kupinga majaribio ya silaha za nyuklia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.Picha ya UM(maktaba)

Baraza Kuu laadhimisha siku ya kupinga majaribio ya silaha za nyuklia

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, leo limefanya kikao cha kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Majaribio ya Silaha za Nyuklia, kikifuatiwa na mjadala kuhusu jukumu la Umoja wa Mataifa katika kutokomeza silaha za nyuklia.

Katika ujumbe uliosomwa na makamu wake, Charles Thembani Ntwaagae, rais wa Baraza Kuu John Ashe amesema azma ya pamoja ya kuhakikisha kuwa silaha za nyuklia zimetokomezwa ulimwenguni ni lazima idhihirishwe katika kujikita katika kupiga rasmi marufuku majaribio ya silaha hizo.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema kutokomeza silaha za nyuklia ni jambo la kipaumbele kwake, na kwamba kutokomeza kufanyia silaha za nyuklia majaribio ni sehemu muhimu.

“Tunapoadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga majaribio ya nyuklia, tuzingatie upya hadithi za manusura. Tusikilize maneno yao, na kuwazia madhara ya ulipuaji wa silaha za nyuklia, kama yangalimfika kila mmoja wetu. Hapo tu ndipo tutaelewa vyema zaidi haja ya kuazimia upya kuwa na ulimwengu usio na silaha za nyuklia na majaribio ya nyuklia.”