Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takwimu mpya zaonyesha kuenea kwa ukatili dhidi ya watoto- UNICEF

UNICEF PHOTO

Takwimu mpya zaonyesha kuenea kwa ukatili dhidi ya watoto- UNICEF

Ukusanyaji mkubwa zaidi wa takwimu kuhusu ukatili dhidi ya watoto unaonyesha kiwango kikubwa cha kuenea kwa utesaji na ukatili wa kingono na kihisia dhidi ya watoto, huku ukibainisha pia mitazamo inayonawirisha na kutoa kisingizio cha ukatili huo na kuuficha katika kila nchi na jamii kote duniani.

Katika ujumbe uliosomwa na naibu wake, Bi Geeta Rao Gupta, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF, Anthony Lake, amesema kuwa takwimu hizo zinasikitisha na kutia aibu

“Hakuna serikali au mzazi atakayetaka kuziona. Hata hivyo, amesema bila kukabiliana na hali halisi ambayo inadhihirishwa na takwimu hizo za ukiukwaji wa haki za mtoto ambaye anapaswa kulindwa, kasumba kwamba ukatili dhidi ya watoto ni jambo la kawaida na linalokubaliwa haitabadilika.”

Ripoti hiyo ya UNICEF iitwayo, Hidden in Plain Sight inatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka nchi 190, ikionyesha ukatili katika maeneo ambayo watoto wanapaswa kuwa salama: katika jamii zao, shule na nyumbani.

Inabainisha pia athari za muda mrefu za ukatili huo, ikionyesha kuwa watoto waliokumbwa na ukatili kama huo huenda wasipate ajira, wanaishi katika umaskini na wanakuwa katili kwa wenzao.