Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajali kazini huua watu Milioni 2.3 kila mwaka duniani: ILO

Picha ya ILO

Ajali kazini huua watu Milioni 2.3 kila mwaka duniani: ILO

Mkutano wa 20 wa kimataifa kuhusu usalama katika mahala pa kazi umeanza leo huko Frankfurt, Ujerumani huku ikielezwa kuwa watu Milioni 2.3 hufariki dunia kila mwaka kutokana na ajali kazini.

Kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), gharama ya ajali kazini na magonjwa yatokanayo na hali hiyo inakisiwa kuwa ni dola Trilioni 2.8.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO Guy Ryder amesema licha ya kwamba takwimu hizo hazikubaliki, bado majanga hayo hayapewi kipaumbele.

Amesema bila shaka kuna mengi yanayohitajika kufanywa kwani ajali kazini siyo tu ni janga la kibinadamu bali pia linagharimu uchumi na jamii.

Mkutano huu ambao hufanyika kila baada ya miaka mitatu unajumuisha wataalamu wa usalama kazini, wanasiasa, na wanasayansi kutoka mataifa 139 na watajadiliana hadi jumatano jioni jinsi ya kufanya mahala pa kazi pawe salama na ya kuzingatia afya.