Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhalifu dhidi ya wasamaria ni ukosefu wa ubinadamu: Eliasson

Jan Eliasson, Picha ya UN

Uhalifu dhidi ya wasamaria ni ukosefu wa ubinadamu: Eliasson

Baraza la usalama limekutana kujadili jinsi ya kulinda maisha ya wasamaria wema katika mizozo, kulingana na maadhimisho ya siku hii ya wasaidizi wa kibinadamu, likijaribu kuelewa sababu za kuongezeka kwa idadi ya wasamaria wanaouawa kila mwaka.  Taarifa zaidi na Abdullahi Boru

(Taarifa ya Abdullahi)

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, amelielezea Baraza la Usalama kusikitishwa sana na ghasia zinazozidi kuathiri wafanyakazi wa usadizi wa kibinadamu, akisema siku hizi waasi wanaopigana kwenye mizozo mbali mbali wanalenga hasa raia wa kawaida na wasamaria wema wakitumia woga kama silaha. Amesema tabia hizo ni ukosefu wa ubinadamu.

“ Ghasia hizo haziathiri tu wasaidizi wa kibinadamu, zinaathiri pia maelfu ya watu ambao hawatafikika tena kwa sababu ya ghasia hizo. Zinaathiri pia watoto ambao hawatapata chanjo, wagonjwa na majeruhi ambao hawatapata matibabu, na waliolazimika kukimbia makwao ambao hawatapata makazi” 

 Eliasson amesisitiza umuhimu wa kutofautisha masuala ya kisiasa na ya kibinadamu, na kuzingatia kutopendelea upande wowote katika vita kama njia ya kutunza heshima za mashirika ya kibinadamu.

Aidha, amelieleza baraza huo kwamba nchi sita duniani zinachangia katika kushambulia wasamaria wema, zikiwemo Afghanistan, Pakistan, Somalia, Sudan, Sudan Kusini na Syria, akiongeza kwamba wahanga wengi ni raia weneyewe wa nchi hizo waliouawa wakati wa kujituma kusaidia wenzao.

Hatimaye, amesema jukumu la baraza la usalama ni la msingi sana katika kusitisha ghasia hizo kwa kukumbusha pande zote za mzozo majukumu yao ya kuheshimu kazi za kibinadamu, kuhakikisha kwamba utaratibu wa kisiasa unaendelea ili kusuluhisha mzozo, na vilevile kuwajibisha watekelezaji wa uhalifu dhidi ya wasamaria wema.