Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha usitishaji mapigano kwa sababu za kibinadamu Gaza

UN Photo/Shareef Sarhan
Robert Serry, Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mashariki ya Kati ziarani Gaza/Picha@

Ban akaribisha usitishaji mapigano kwa sababu za kibinadamu Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha hatua iliyochukuliwa mapema leo na Israel kusitisha mapigano kwa muda wa saa tano ili kuruhusu shughuli za kibinadamu kwa raia wa Gaza, zikiwemo usambazaji misaada na kufanyia ukarabati miundo mbinu muhimu kama umeme na maji. Usitishaji mapigano huo uliotokana na juhudi za upatanishi za Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa Mashariki ya Kati, Robert Serry, na ambao ulifanyika kati ya saa nne asubuhi na saa tisa alasiri, uliwawezesha pia raia wa Ukanda wa Gaza angalau kupata afueni kutokana na mashambulizi ya roketi.

Bwana Serry amesisitiza umuhimu ya kukomesha mapigano kabisa, na yafanyike mazungumzo ili kupata suluhu kwa mgogoro huo wa Gaza.

Wakati huo huo, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limechukua fursa hiyo kutoa misaada ya dharura kwa maelfu ya waathiriwa ambao wamekumbwa na upungufu wa chakula katika ukanda wa Gaza. WFP imesema mahitaji ya chakula ni ya dharura kwa raia walioathiriwa na mzozo katika Ukanda wa Gaza.