Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan yashutumiwa kuwarejesha wakimbizi na waomba hifadhi kwa lazima

Wkimbizi wa Eritrea: Picha ya UNCHR

Sudan yashutumiwa kuwarejesha wakimbizi na waomba hifadhi kwa lazima

Raia wa Eritrea wapatao 74 waliokwenda Sudan kuomba hifadhi wameondolewa kwa lazima na kurejeshwa nyumbani, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR.

Watu hao walirejeshwa Eritrea mnamo Jumatatu ya tarehe 30 Juni.

UNHCR imesema kuwa waomba hifadhi hao walikuwa wameshtakiwa na kuhukumiwa kuingia Sudan kinyume na sheria, lakini hawakupewa fursa ya kufikia vyombo vya kusaidia katika harakati za kuomba hifadhi ili madai yao yatathminiwe na watu wenye uwezo.

UNHCR imeelezea kusikitishwa na vitendo hivyo vya Sudan kuwarejesha kwa lazima wakimbizi na waomba hifadhi wa Eritrea

Msemaji wa UNHCR, Melissa Fleming, amesema kuwa kuwarejesha wakimbizi kwa lazima ni ukiukwaji mkubwa wa mkataba kimataifa wa mwaka 1951 kuhusu wakimbizi, na sheria ya Sudan ya 2014 kuhusu waomba hifadhi salama.  Amesema UNHCR inaikumbusha serikali ya Sudan kuhusu wajibu wake chini ya mkataba wa kimataifa na katiba ya Sudan, na kutoa wito kwa mamlaka kuwawezesha waomba hifadhi kufikia vyombo vya kuwasaidia, na kuwalinda kutokana na kurejeshwa nyumbani.

Kuna zaidi ya wakimbizi na waomba hifadhi 160,000 nchini Sudan, wakitoka Eritrea, Ethiopia, DRC, Chad na Sudan Kusini.