Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wahimiza utulivu baada ya mauaji ya vijana Israel

Picha@Ravina Shamdasani/OCHR

UM wahimiza utulivu baada ya mauaji ya vijana Israel

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, imepigwa na huzuni baada ya miili ya wavulana watatu wa Israel walioripotiwa kupotea hapo tarehe 12 Juni kupatikana wakiwa wameuawa katika Ukingo wa Magharibi. Ofisi hiyo imetoa rambirambi zake kwa jamii za wavulana hao na kutaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahalifu wa mauaji hayo. Taarifa zaidi na John Ronoh

Imefahamika kwamba hapo jana uskiku, wapalestina 6 walijeruhiwa na wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi. Ofisi ya Haki za Binadamu imebaini kuwa kumekuwa na mashambulizi ya roketi kutoka Ukanda wa Gaza na pia mashambulizi kutoka angani na kwa bahari, yakitekelezwa na vikosi vya wanajeshi wa Israel mjini Gaza. Kumekuwepo pia kuzuia raia kutembea na mapigano kwenye makazi katika Ukingo wa Magharibi.

Ofisi ya haki za binadamu imezihimiza pande zote husika kuheshimu sheria za kimataifa ili kuzuia mauji, majeruhi na vitendo vyote vya ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba wote wasiendelee kuumiza raia kwa makosa ambayo hayajasababishwa na raia hao binafsi. Ravina Shamdasani ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu.

“Tunatoa wito kwa Waisraeli na Wapalestina wote kujizuia, na kuzuia hali kuzorota zaidi. Usiku uliopita, kijana mmoja wa Kipalestina aliuawa, na kuifanya idadi ya Wapalestina waliouawa Ukingo wa Magharibi kufikia saba, wakiwemo vijana 3, tangu Juni 12. Tunatuma rambi rambi zetu kwa familia zao zote.”