Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakazi wa Rakhine wazidi kukumbwa na manyanyaso safarini, UNHCR yaingia hofu

Mmoja wa wakazi wa Rakhine baada ya kuwasili Malyasia kufuatia safari ndefu baharini. (Picha© UNHCR/B.Baloch)

Wakazi wa Rakhine wazidi kukumbwa na manyanyaso safarini, UNHCR yaingia hofu

Miaka miwili baada ya mapigano ya kikabila kwenye jimbo la Rakhine huko Myanmar, maelfu ya wakazi wa eneo hilo wanaendelea kukimbia kwa kutumia mashua kupitia pwani ya Bengal ambako ripoti za manyanyaso na utumikishwaji zinawakumba kila uchao.

Hali hiyo inatia hofu shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, likikadiria kuwa zaidi ya watu Elfu Themanini na Sita wengi wao wa kabila la Rohingya, wamekimbia makwao kwa kutumia usafiri wa mashua tangu Juni mwaka 2012 ikiwemo 15,000 mwaka huu pekee.

Hata hivyo wakati wanasaka usalama, bado wanakumbwa na manyanyaso wakiwa safarini au huko wafikako ambapo baadhi yao waliofanikiwa kufika Thailand, Malaysia au Indonesia wameiambia UNHCR kuwa mashua huwa zimejaa watu kupindukia, hawana chakula cha kutosha au maji kutokana na kuwepo baharini muda mrefu. Wanaofariki dunia wakiwa safarini hutoswa baharini.

UNHCR imetaka taratibu za mpito za makazi kwa wananchi hao hadi pale hali ya utulivu itakaporejea kwenye jimbo la Rakhine.