Mauaji ya mwanamke mjamzito Pakistan: serikali ichukue hatua, UM waonya

28 Mei 2014

Kufuatia kitendo cha mwanamke mjamzito nchini Pakistani kupigwa mawe hadi kuuawa tarehe 27 mwezi huu, Navi Pillay, ambaye ni Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, amelaani vikali kitendo hiki na kuiomba serikali ya Pakistan ichukue hatua kuzuia mauaji kama hayo.

Mwanamke huyo Farzana Parveen aliyekuwa na umri wa miaka 25 alipigwa mawe ndugu zake 20 akiwemo baba yake na kaka zake wakati akielekea mahakamani na mume wake kujibu mashtaka yaliyofunguliwa na baba yake dhidi yake ya kwamba ametekwa nyira na mume wake na ndoa yao ni haramu.

Navi amesema amesikitishwa sana na kifo cha Farzana ambaye, kama wanawake wengi nchini humo, ameuawa na familia yake, kwa msingi wa kuolewa na mwanaume aliyemchagua mwenyewe.

Kwa mujibu wa kamati ya haki za binadamu ya Pakistan, wanawake 869 wameuawa mwaka jana kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kuolewa kinyume na maamuzi ya familia zao, mauaji hayo yakiitwa mauaji ya “heshima”.

Pillay amesema, hakuna heshima yeyote katika mauaji hayo, na amesikitika kuona kwamba mara nyingi watekelezaji hawakamatwi ama hawapewi adhabu za kuonekana. Ameongeza ni jukumu la serikali kupeleka watekelezaji mbele ya sheria, na kuhakikisha kamba wanawake kama Farzana wanapewa usalama wa kutosha.

Pakistan ina kiwango cha juu zaidi duniani cha ukatili dhidi ya wanawake.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter